Mama yako mzazi yu mgonjwa mahututi katika hospitali ya Wilaya ya Masasi. Madaktari wamelifahamu tatizo lake lakini hakuna vifaa wala wataalamu wa jinsi ya kumtibu. Anatakiwa ahamishiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako kuna madaktari bingwa na vifaatiba vya uhakika. Hata hivyo safari ya kutoka Masasi hadi Dar Es Salaam, pengine yaweza... kupoteza uhai wake.
Lakini usihofu... Tanzania sasa imepata neema
baada ya kuwepo kwa huduma ya Tiba kwa njia ya Teknolojia ya habari na
mawasiliano, kwa kitaalamu ‘telemedicine’
Telemedicine ni utoaji wa huduma za afya au
mbadilishano wa taarifa za kitiba kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa
kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano.
Mafanikio ya uvumbuzi huu yamesaidia wataalamu wa afya kubaini na kutibu wagonjwa bila kuonana nao uso kwa uso.
Kwa kifupi, unaweza ukazungumza na daktari wako na
kumweleza vile unavyojisikia, kisha akakuandikia vipimo, na baada ya
kumpa majibu ya vipimo hayo kwa njia ya teknolojia pia, atakuandikia
dawa au kukupa ushauri wa kitiba.
Pia, Hospitali yenye vifaa na wataalamu wanaweza
kuzungumza na madaktari katika hospitali za vijijini na kutoa ushauri wa
jinsi ya kumtibu mgonjwa aliye taabani.
Hivi sasa hospitali nne nchini zimeunganishwa
katika mradi huo wa Telemedicine ambazo ni Mwananyamala, Amana, Temeke
na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH) pamoja na hospitali ya Tumbi,
Mkoa wa Pwani.
Mei, 2011 ndiyo wakati ambao Rais Jakaya Kikwete
alizindua mradi huu akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa India, Dk
Manmohan Singh.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Modou Gaye anasema teknolojia hii
inawezesha madaktari walioko katika Hospitali za Amana, Mwananyamala,
Temeke, Tumbi na Bagamoyo kuwasiliana moja kwa moja na madaktari bingwa
pamoja na watalaamu wengine walioko Muhimbili katika kujadili,
kushauriana na hatimaye kufanya uamuzi kuhusiana na tiba, uchunguzi wa
mgonjwa husika.
Gaye anasema kuwa teknolojia hii itamwezesha mgonjwa aliyeko kati ya hospitali hizo kupata matibabu bila kufika Muhimbili.
Anasema kupitia teknolojia hii wataalamu wataweza
kuwasiliana katika nyanja za ushauri, vipimo vya uchunguzi mathalan vya
radiolojia, vipimo vya uchunguzi vya patholojia, magonjwa ya moyo na
mafunzo kwa watalaamu.
Uwepo wa teknolojia hii utawezesha mgonjwa
anayehitaji kupata huduma za kibingwa Muhimbili kutibiwa haraka na kwa
muda mfupi kuliko ambayo angefuata utaratibu wa rufaa na hivyo
kumpunguzia muda wa kukaa hospitalini kwa muda mrefu.
>>>MWANANCHI
>>>MWANANCHI